Posted on 2018-04-13 05:17:56

Juzi kulikua na mchezo wa kirafiki kati ya chuo changu ‘MSJ’ na moja ya taasisi ilio jirani,baadhi ya rafiki zangu wakawa wakijinadi na kujigamba kuwapiga 4G wale mabwana,inafurahisha na imekua ni neno la kawaida sana hasa kuonesha dhihaka kwa timu pinzani lakini je watu wanajua nini kuhusu kitu hiki?kiasi kua ukiwauliza walio wengi utakosa jibu sahihi
          Herufi zinazoonekana katika eneo la mnara wa mtandao katika vioo vya simu zetu ni vifupi vya vizazi (Generation) vya mtandao husika na kwa sasa tuna 4G, H+, H, 3G, E (Edge), G (Gprs) na kwa wale watumiaji wa Blackbery kuna alama ya BB kama utakuwa unatumia Blackberry Internet Service maarufu kama BIS. Tunatumia data katika kutuma na kupokea barua pepe, kusikiliza na kupakua miziki, video pamoja na picha mtandaoni.

           Hivi vyote ni vizazi vya Wireless Network (mtandao usiotumia waya) na tofauti kubwa ni kasi ya kupandisha na kupakua data (uploading and downloading speed). Teknolojia hizi hutegemea sana aina ya simu, na kampuni ya simu inayotoa huduma ya mtandao. Kwa mfano, unaweza ukawa na simu yenye uwezo wa kukamata 4G ila mtandao unaotumia ukawa hautoi huduma hii

          GPRS (General Packet Radio Service)Hiki ni teknolojia ya kwanza katika kizazi cha pili cha network, 2G (Second Generation), teknolojia hii ina uwezo wa kasi ya kupakua (download speed) mpaka 171Kbps (Kilobits per second) kama kasi ya juu kabisa ya kupakua. Nchini teknolojia hii ilikuwepo sana kipindi cha miaka ya 2000 wakati mitandao ya simu za mkononi ilipoanza kuingia kwa kasi japo wa sasa GPRS haina nafasi sana katika mitandao yetu kwa sababu kasi yake ni ndogo sana ukilinganisha na mitandao vizazi vingine kwa sababu mapungufu ya teknolojia hii ni kasi ndogo ya kupakua data pamoja na kutokuwa na uwezo wa kupiga simu na kutumia data kwa wakati mmoja.

          EDGE (Enhanced Data GSM Evolution)GPRS na EDGE vyote ni vizazi vya 2G ila EDGE ina kasi kubwa zaidi ya kupakua (download) ukilinganisha na GPRS. EDGE na GPRS zikiunganishwa huwa zinaitwa 2.5G Networks na inakuwa na kasi zaidi. Hapa nchini kwetu kabla ya mwaka 2014 mitandao karibia yote ya simu ilikuwa inatoa huduma hii, na huwa inawakilishwa na heri E au EDGE katika mnara wa network.

           3G (Third Generation Network) Kuja kwa 3G kumefanya kuangalia video mtandaoni iwe rahisi au kupiga simu za video, ni mtandao wenye kasi ya wastani na karibia mitandao yetu yote ya simu inatoa huduma hii kwa sasa hasa maeneo ya mijini. Mtandao huu una kasi ya kupakua mpaka 3.1 Mbps na ulianza kutumika rasmi mwaka 2001,kama unakumbuka vodacom ndio walikuwa wa kwanza kuleta teknolojia hii hapa nchini na tangazo lao la George Poji na Amanda (Natania jamani!)

          HSDPA (High-Speed Down-Link Packet) Hiki bado ni kizazi cha tatu cha mtandao (3G) kilichoongezewa nguvu na kuwa na kasi ya kupakua mpaka 14Mbps na muda mwingine hufahamika kama 3.5G . Mara nyingi kwenye simu zetu huwa inawakilishwa na herufi H, na kama nitakua sikosei Airtel walikuwa wa kwanza kujinadi kwa teknolojia hii hapa nchini.

          HSPA+ (Evolved High-Speed Packet Access) HSPA+ ni muendelezo wa HSPA(HSDPA&HSUPA), ni mtandao wenye kasi zaidi na ni mwanzilishi wa kizazi cha nne cha mtandao (4G). HSPA+ inauwezo wa kupakua mpaka wastani wa 168Mbps kasi kubwa zaidi ya vizazi vyote vilivyopita na huwa inawakilishwa na H+ katika simu zetu.

          4G LTE (Long Term Evolution) LTE ni kizazi cha 4 cha mtandao (4G) kinachosapoti kustream (kuangalia mtandaoni) video za HD (High Definition) au video zenye ubora wa juu kabisa kwa kuwa teknolojia hii ina kasi mpaka ya 299.6Mbps kasi kubwa zaidi kwa sasa. Mitandao kama Smile na Tigo kwa sasa wameshaanza kutoa huduma hii kwenye baadhi ya maeneo nchini.

          Kampuni ya kutengeneza simu ya Samsung Electronics yenye makao makuu yake nchi Korea Kusini tayari wameanza kufanya majaribio ya kizazi cha tano cha mtandao, 5G japo haijatangaza rasmi lini teknolojia hiyo itaingia mtaani.

          Nadhani nitakuwa nitakuwa nimesaidia kwa namna moja au nyingine katika kutoa elimu ya teknolojia hii na kuwafanya wale wanaowadhihaki wenzao kuhusu 4G kujua maana yake.